

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepata ahueni katika maandalizi ya timu ya taifa 'Taifa Stars' kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya uongozi wa Hoteli ya White Sands kugharamia kambi ya timu hiyo hapa nchini kabla ya kuelekea Misri katika fainali hizo.Stars itaweka kambi ya siku sita kwenye hoteli hiyo na baada ya Juni 7 itaelekea Cairo, Misri ambako itaweka kambi nyingine hadi Juni 21 ambapo fainali hizo zitaanza rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Motisun Group, Subhash Patel alisema wameamua kugharamia kambi hiyo ya Stars pindi ikiwa hapa nchini kutokana na thamani na ukubwa wa mashindano ya AFCON.
"Ni miaka 39 imepita tangu Taifa Stars iliposhiriki Fainali za AFCON wengine tulikuwa vijana na baadhi walikuwa hata hawajazaliwa hivyo kushiriki mashindano hayo ni jambo la kipekee na lenye maana.
“Kwa kulitazama hilo uongozi wa Motisun Group tumeona Taifa Stars iweke kambi pasipo gharama yoyote kwenye hoteli yetu ya White Sands kwa muda wote itakapokuwa inafanya maandalizi hapa nchini tukiamini kwamba hiyo itasaidia kuleta chachu kwa wachezaji kufanya vizuri kwenye hayo mashindano," alisema Patel.
Rais wa TFF, Wallace Karia alisema shirikisho hilo limepokea kwa mikono miwili ofa hiyo na akaomba wadau wa soka kuiga kile kilichofanywa na Motisun Group.
"Tunamshukuru sana Mzee Subhashi kwa kuitikia wito wa serikali yetu katika kuinua michezo. Hii sio mara ya kwanza kwani alitusaidia kwenye mashindano yaliyopita ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17).
Mzee wetu kupitia kampuni yake ta Motisun Group ametupa ofa ya kukaa kwenye hoteli ya White Sands kwa kipindi chote cha kambi hapa nchini. Hili ni jambo zito kama mnavyojua tupo kwenye kipindi kigumu kama shirikisho bado hatujapokea fedha za maandalizi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) alisema Karia.
Jumla ya wachezaji 39 ambao kocha wa Stars, Emmanuel Amunike amewaita kwenye kikosi cha awali, wataingia kambini kwenye hoteli hiyo na baada ya hapo saba watatemwa kabla ya safari ya Misri.



0 Comments