Windows

Inbar Yaitaka Tanzania Kuwekeza Mkazo Biashara Ya Mianzi

Na Grace Semfuko, MAELEZO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Kimataifa la Kuendeleza na Kusimamia Biashara ya Mianzi (INBAR) limesema ipo haja kwa Serikali ya Tanzania kutunga Sera zitakazoweza kuhamasisha wakulima hapa nchini kulima zao hilo ambalo pamoja na kuhifadhi Mazingira pia lina tija kiuchumi.
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam jana Jumamosi (Mei 11, 2019) Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Balozi Ali Mchumo alisema ni muhimu kwa nchi ya Tanzania kuzalisha zao hilo ili kuongeza uchumi kutokana na kuwa na soko la uhakika hasa kwa nchi zilizoendelea.
 
“Soko la zao la Mianzi ni kubwa sana Duniani, nawasihi wakulima wazalishe kwa wingi kwani kwenye mataifa mengine wanatumia mpaka kuendeshea mitambo ya viwanda,ndege, kuhifadhi mazingira pamoja na ujenzi, zao hili lina faida kubwa tusilidharau” alisema Balozi Mchumo.
 
Alisema kuna aina zaidi ya 1,600 za mianzi Duniani na zote hizo zikiwa na ubora wa hali ya juu hivyo uzalishaji wa zao hilo kwa Tanzania hautakosa soko na kwamba Shirika lake limejikita katika kuhamasisha na kutafuta masoko.
 
Balozi Mchumo aliwatoa wasiwasi wakulima wa Tanzania kuhusiana na kuzalisha zao hilo kwa kusema kuwa ni rahisi, halina gharama kubwa katika utunzaji wake na lina faida kubwa kwenye soko la Dunia kwani nchi nyingi hasa zenye matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara hutumia mianzi katika kujengea nyumba zao.
 
Aliongeza kuwa kwenye fukwe za Bahari zao hilo limekuwa likihifadhi mmomonyoko wa ardhi kutokana na mizizi yake kushikamana na hivyo kuondoa kabisa athari za kimazingira.
 
Aidha Balozi Mchumo alizitaja sifa za mmea huo kuwa ni pamoja na kustawi kwa haraka kwa kipindi cha  miezi nane hadi tisa mpaka kufikia matumizi yake, ni mgumu kuvunjika au kuoza na ni mwepesi kuubeba, unahifadhi mazingira na kwamba  unafaa kwa ujenzi, na pia unatumika kutengeneza sakafu za majumbani na sehemu nyinginezo inatumika kutengenezea samani za majumbani na maofisini.
 
Akifafanua zaidi Balozi Mchumo alisema Shirika hilo lina nchi wanachama zaidi ya 45 katika Bara la Asia na Afrika ambapo wameuona umuhimu wa kuendeleza na kusimamia biashara ya mianzi Duniani inayotajwa kuwa na tija kiuchumi na kimazingira na hivyo kuwahamasisha mataifa ya nchi wanachama kuzalisha kwa wingi zao hilo. 
 
Inakadiriwa kuwa Duniani kote eneo ambalo linalooteshwa mianzi ni zaidi ya hekta Bilioni 30 huku Barani Asia pekee zao hilo linaliingizia zaidi ya dola Bilioni 60 kwa mwaka kutokana na matumizi mbalimbali ya zao hilo.
MWISHO.





Post a Comment

0 Comments