Ndio, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ipo kwenye mtihani mzito mbele ya Mtibwa cha kuhakikisha wanaifungia timu yao mabao ya kutosha ili iweze kuvuka salama kipindi hiki wanachokabiliwa na presha ya ubingwa inayoletwa na watani zao Yanga.
Ni mabao na ushindi tu vinavyoweza kuweka sawa hesabu zao za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwani vinginevyo watazidi kujiweka kwenye hali ngumu ikiwa watapoteza au kutoka sare kwenye mchezo huo.
Ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 82, Simba baada ya mchezo wa leo itakuwa imebakiza mechi nne na kati ya hizo, mbili ni za ugenini hivyo inaweza kujiweka kwenye hatari ya kutibua hesabu zake kama itafungwa na kuwapa nafasi Yanga ambao kama wanashinda mechi zao mbili zilizobaki watafikisha pointi 89.
Lakini mbali na kuipunguzia presha timu yao, washambuliaji wanapaswa kuitumia mechi dhidi ya Mtibwa leo, kumaliza mkosi uliowaandama katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar waliyopoteza kwa bao 1-0 na ile ya Azam waiyotoka sare ya bila kufungana.
Safu ya ushambuliaji ya Simba inaonekana kukosa ubunifu wa kutumia vyema nafasi ambazo timu hiyo inatengeneza ndani ya eneo la hatari la wapinzani, kufumania nyavu na udhaifu huo kama utatumiwa vyema na Mtibwa wanaweza kuwashangaza Simba leo.Lakini pamoja na hilo, safu ya ulinzi ya Simba nayo imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara hasa ya kutokuwa na mawasiliano mazuri baina ya mabeki au na kipa wao Aishi Manula yamekuwa yakiwagharimu mara kadhaa kwa kuzisaidia timu pinzani kuwatungua.
Ingawa ina udhaifu huo, uimara wa Simba bado unabakia kwa safu yake ya ushambuliaji inayoundwa na nahodha John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao kwa pamoja wamefunga jumla ya mabao 48 katika mechi 33 walizocheza msimu huu.
Mtibwa wao nguvu yao kubwa iko pembezoni mwa uwanja ambako ndiko kumekuwa kukizalisha mabao ya timu hiyo kutokana na uwepo wa mawinga wenye kasi, akili na wenye uwezo mkubwa wa kuwalisha washambuliaji wa timu hiyo.
Udhaifu wa Mtibwa ni udhaifu wa safu yao ya ulinzi ambayo imekuwa haichezi kwa nidhamu na imekuwa na makosa ya mchezaji mmoja mmoja ambayo yamekuwa yakitoa faida kwa wapinzani.
Nje ya Uwanja, rekodi baina ya timu hizo mbili zinaiweka kwenye hali nzuri Simba, kisaikolojia kwenye mchezo wa leo kwani imekuwa ikipata matokeo mazuri pindi ikutanapo na Mtibwa ambayo haijapata ushindi dhidi yao kwa muda mrefu.
Katika mechi 10 za Ligi Kuu ambazo zimekutanisha timu hizo kwenye misimu mitano iliyopita, Simba imeibuka na ushindi mara sita na zimetoka sare mara nne na Mtibwa haijawahi kuibuka na ushindi hata mara moja.
Kwenye mechi hizo, Simba imefunga jumla ya mabao 11 huku ikiruhusu Mtibwa wafumanie nyavu zao mara tatu na katika kuonyesha ni kwa namna gani nyavu zimekuwa zikiteseka pindi timu hizo zinapokutana, ni mara moja tu kati ya mechi hizo 10 za Ligi Kuu ambazo wamekutana, iliyomalizika bila bao kufungwa.
Ni muda wa miaka sita na miezi miwili (siku 2273) ambao umepita tangu Mtibwa Sugar walipopata ushindi kwa mara ya mwisho dhidi ya Simba walipoichapa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu msimu wa 2012/2013 uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, Februari 24,2013.
Tangu hapo Mtibwa wamekuwa wanyonge wa Simba na licha ya kuwa wameshajinusuru kushuka daraja, mchezo wa leo ni muhimu kwao kumaliza mkosi wa kutopata matokeo mazuri kwa muda mrefu dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.
SIKIA TAMBO SASA
Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila alisema mchezo wa leo dhidi ya Simba ni muhimu kwao ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza katika nafasi ya nne.
“Hadi sasa wachezaji wote wako sawa hamna majeruhi yeyote ambaye anaweza kukosa mchezo wa kesho (leo).
Tunauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huu ili tuweze kujiweka kwenye nafasi yetu ikumbukwe kwamba KMC wameshinda hivyo tumeshushwa kwa nafasi moja lakini tukishinda tunarudi pale.
Kikubwa tunacheza na Simba tunafahamu Simba wapoje na wanachezaje na tunajua kwamba wana wachezaji wenye uchu hivyo tumejipanga kukabiliana nao,” alisema Katwila.
Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema wamejiandaa vyema kimbinu na kisaikolojia kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wa leo.
“Mchezo uliopita dhidi ya Azam tulicheza vizuri lakini bahati haikuwa kwetu na kama ulivyoona wenzetu walilinda vizuri na kwa bahati mbaya sisi tukashindwa kutumia nafasi tulizopata.
Mchezo dhidi ya Mtibwa tumejipanga vizuri kuhakikisha kwanza tunakuwa na kiwango bora kama ilivyokuwa dhidi ya Azam, lakini tunawajenga kisaikolojia wachezaji wetu mechi mbili zinazofuata ni za kufa au kupona. Wachezaji wote wamefanya mazoezi na wako tayari kwa mchezo kutegemea na mapendekezo ya kocha kasoro Juuko na Kapombe ambao hawapo,” alisema.
0 Comments