MKURUGENZI wa Kampuni ya Motisun Group na Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Subhash Patel, amenogesha kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya kutoa siku sita za kukaa katika Hoteli ya White Sand, Dar es Salaam.

Kambi hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya Stars kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazoanza Juni 21 mwaka huu, nchini Misri.

Stars ambayo imepangwa Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya, Harambee Stars, itaanza kutupa karata yake ya kwanza katika michuano hiyo kwa kumenyana na Senegal Juni 23, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Walace Karia, alisema timu inatarajia kuingia kambini Juni mosi ambapo itakaa kwa muda wa siku sita kabla ya kwenda Misri Juni 7, mwaka huu.

“Tunamshukuru ndugu yetu Patel kwa mchango wake wa kusaidia michezo, ametupatia kambi katika moja ya hoteli inayomilikiwa na kampuni zake, White Sand, ambako timu itakaa kwa siku sita, bajeti iliyokuwa itumike kwa ajili hiyo itaweza kusaidia mambo mengine.

“Ni vizuri watu wengine wafuate nyayo zake kusaidia soka, wachezaji 40 kukaa kuweka kambi katika hoteli kama hiyo ni jambo kubwa, tunamshukuru na tunaamini hali hii itaisaidia timu yetu kuwa na morali ya kufanya vizuri,” alisema Karia.

Aidha, alisema timu ikiwa nchini itacheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Misri na pia wapo katika mazungumzo na timu nyingine kati ya Zimbabwe na Nigeria.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Motisun Group, Patel alisema kwa muda mrefu timu hiyo haijashiriki michuano ya Afcon, hivyo ni vyema kuwapa sapoti ili waweze kufanya vizuri.

“Nafasi hii ni fahari kubwa kwa Tanzania hivyo ni vizuri kuungana kwa lolote ambalo tunaweza kusaidia ili tuwape motisha wachezaji, wakiwa hotelini wanaweza kupata fursa ya kufundishwa hata kwa kutumia kompyuta,” alisema Patel.

Alisema kocha ataondoka na wachezaji 32 kwenda Misri lakini kambi rasmi kwa ajili ya Afcon watabaki wachezaji 23, pia mwalimu ataangalia wale watakaoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ambazo zitafanyika muda mfupi baada ya Afcon.

Stars ilifuzu kucheza fainali hizo baada ya kuwafunga vinara wa Kundi L Uganda, The Cranes, mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam, hivyo kufikisha pointi nane ikishika nafasi ya pili.