UONGOZI wa Lipuli FC umesema kuwa safari yao ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho imewadia kwani wamejipanga kukabiliana na Yanga hatua ya nusu fainali kutokana na wengi kudai kwamba walibahatisha ushindi wao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Lipuli walitinga nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kuifunga Singida United mabao 2-0, huku Yanga ikiifunga Alliance kwa penalti 4-3. Sasa zitakutana kwenye Uwanja wa Samora kuwania kutinga fainali.
Kocha wa Lipuli, Seleman Matola amesema ilikuwa ni dua ya timu tangu mwanzo wa hatua ya robo fainali kukutana na Yanga na imetimia hivyo kinachofuata ni kichapo tu.
"Ilikuwa ni dua japo tulijipanga pia kwa ajili ya kucheza na Alliance ila tulikuwa tunaitamani sana Yanga yenyewe ya Mwinyi Zahera ili tuwanyooshe tena mara ya pili kisha tusonge mbele hatua ya fainali.
"Malengo yetu ni kuona namna tutakavyofanikiwa kutwaa ubingwa huu kwani hakuna mwalimu anayefikiria kushindwa, nawatambua vizuri Yanga, mbinu zao nazitambua hivyo hakuna kinachoniogopesha lazima tupambane kupata matokeo chanya," amesema Matola.
0 Comments