UONGOZI wa Klabu ya Yanga umekutana katika mwendelezo wa vikao kujadili juu ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo.
Kikao hicho kilifanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, juzi kilikuwa chini ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na viongozi mbalimbali wa soka hapa nchini akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Leodegar Tenga.
Awali, Klabu ya Yanga ilitarajiwa kufanya uchaguzi wake Januari 13, mwaka huu kuziba nafasi za baadhi ya viongozi waliojiuzulu ndani ya klabu hiyo akiwemo Mwenyekiti, Yusuf Manji pamoja na makamu mwenyekiti Clement Sanga na baadhi ya wajumbe mbalimbali, uchaguzi ambao ulivunjika kutokana na baadhi ya wanachama kuupeleka mahakamani.
Yanga kwa sasa ipo katika mchakato wa kuandaa uchaguzi kwa ajili ya kuchagua viongozi wapya ndani ya klabu hiyo ambapo kwa sasa vikao vinaendelea.
Mwakyembe alisema walikuwa na kikao kwa ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali ya uchaguzi wa Yanga ambapo pande zote mbili wameonekana kukubali kufanya uchaguzi.
“Juzi viongozi mbalimbali wa soka wa TFF na BMT walikutana na mimi nikaona ni vyema nikajiunga nao kwa ajili ya kujadili suala la uchaguzi wa Klabu ya Yanga.
“Mambo yanaonekana kwenda vizuri na kwa bahati nzuri kila mmoja anaonekana kuhitaji uchaguzi kufanyika hakuna malumbano hata kidogo, uchaguzi utafanyika wakati wowote kuanzia sasa ambapo kuna taratibu tu tunaendelea kuzifanya.
“Tumekuwa na vikao endelevu baada ya hapo tutakaa tena siku nyingine baada ya siku mbili tatu hadi tufikie muafaka, kwani kuna baadhi ya vitu tunavirekebisha ili twende sawa, kwa sasa tunaangalia zaidi mechi ya Taifa Stars,” alisema Mwakyembe.
0 Comments