Kadi mbili nyekundu, makocha wote wawili wakatimuliwa uwanjani. Lakini licha ya hayo yote, Gor Mahia walimudu kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miongo miwili. Gor waliwafunga Petro Atletico ya Angola 1 – 0 katika mtanange wa mwisho wa makundi katika dimba la Moi Kasarani jijini Nairobi Jumapili usiku.
Na wakati kipyenga cha mwisho kilipopulizwa, mashabiki wa Gor walimiminika katikati mwa uwanja mithili ya nyuki ili kuwa sehemu ya tukio hilo la kihistoria.
Bao la Gor lilipatikana kupitia mkwaju wa penalti uliosukumwa wavuni na mchezaji Mnyarwanda Jacques Tuyisenge.
“Tunapaswa kuwapongeza vijana kwa kucheza vizuri licha ya kuwa pungufu uwanjani kwa kipindi kirefu,” alissma kocha wa Gor Hassan Oktay ambaye pia alitimuliwa uwanjani baada ya kukosa nidhamu pamoja na wachezaji wake Ernest Wendo na Shafiq Batambuze.
Na hizi ndizo timu 8 zilizofuzu Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
RS Berkane
CS Sfaxien
Al Hilal Club
Zamalek SC
Hassania Agadir
Etoile Sahel
Nkana FC
Gor Mahia FC
Droo itakuwa Jumatano Machi, 20.
0 Comments