Turin, Italia. Supastaa, Cristiano Ronaldo ni mchezaji aliyezoea kubeba mataji mbalimbali yanayopiganiwa kwenye soka.
Hadi sasa taji kubwa ambalo hajawahi kubeba ni Kombe la Dunia tu, lakini mengine yote tayari, ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya alilobeba mara kibao. Huko kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiko Ronaldo anakoonyesha kwamba yeye ni balaa kubwa.
Msimu huu kwenye hatua ya robo fainali timu yake mpya Juventus imepangwa kumenyana na Ajax, ambao suala la kuwafunga kwake imekuwa kitu chepesi kama kumeza mate tu.
Kwenye michuano ya Ulaya, Ronaldo ana timu zake anazozitesa kwenye michuano hiyo ya Ulaya, anapokutana nazo kwa kuzifunga mara nyingi. Hizi hapa ndio timu ambazo Ronaldo amezitesa kwa kuzifunga mara nyingi kwenye michuano ya Ulaya ikiwamo Ajax Amsterdam.
5. Ajax – mabao 7
Ajax waliwatupa nje Real Madrid kibabe kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, lakini kwa bahati mbaya wamepangwa na Ronaldo kwenye mechi ya robo fainali, mchezaji ambaye amekuwa na kawaida ya kuwafunga sana. Kwenye hatua ya robo fainali, Wadachi hao wamepangwa kuwakabili Juventus, ambao ndiyo waliomwaajiri Ronaldo kwa sasa baada ya kumtoa huko Real Madrid. Huko nyuma, Ronaldo alikutana na Ajax kwenye mechi za makundi tu, ambapo kwenye msimu wa 2010/11, ambapo alifunga mabao kwenye mechi zote mbili, akifunga mara saba na kuasisti mara mbili.
4. Borussia Dortmund – mabao 7
Borussia Dortmund ilikuwa timu ngumu sana kwa Real Madrid. Lakini, Ronaldo wala hakuwa na ugumu wowote kwenye mechi alizokutana na Wajerumani hao kwenye michuano ya Ulaya, kwani ni miongoni mwa timu alizozifunga mara nyingi. Katika msimu wa 2012/13, Real Madrid ilikutana na Dortmund mara nne, Ronaldo akafunga bao moja katika mechi ya hatua zote za hatua ya makundi na kwenda kufunga jingine kwenye nusu fainali. Msimu uliofuatia walikutana tena na Ronaldo alifunga bao kwenye ushindi wa 3-0 katika robo fainali. Katika msimu wa 2016/17 na 2017/18 walikutana tena kwenye hatua za makundi na Ronaldo amefunga mara nne katika mechi nne alizowakabili.
3. Atletico Madrid – mabao 7
Jumanne iliyopita, Atletico Madrid walisambaratishwa tena na Ronaldo, wakati alipowapiga mabao matatu na kuwasukuma nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye hatua ya 16 bora. Mabao hayo matatu yamemfanya Ronaldo kufikisha saba ambayo amewafunga Atletico katika mechi alizokutana nao kwenye michuano hiyo ya Ulaya. Mara ya kwanza kuwafunga ilikuwa kwenye fainali ya michuano hiyo msimu wa 2013/14. Misimu miwili iliyofuatia, hakuwafunga, kabla ya kuja kuwapiga hat-trick kwenye nusu fainali msimu wa 2016/17 na kika kuja kuwafunga tatu nyingi Jumanne iliyopita, safari hii akiwa na Juventus.
2. Bayern Munich – mabao 9
Bayern Munich na Real Madrid ni timu mbili zenye rekodi nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na jambo hilo zimelifanya timu hizo kuwa mahasimu wakubwa wanapokutana uwanjani. Lakini, wababe hao wa Ujerumani ni miongoni mwa wahanga waliofungwa mara nyingi na supastaa Ronado katika mechi za michuano hiyo ya Ulaya. Katika nusu fainali ya 2011/12, Ronaldo alifunga mara mbili kwenye mechi ya marudiano, lakini alishindwa kuifikisha timu yake fainali. Msimu wa 2013/14, alirudia yake makali yake akifunga mara mbili pia kwenye nusu fainali ya pili. Misimu mitatu baadaye walikutana kwenye hatua ya robo fainali na Ronaldo alifunga mabao matano katika mechi mbili walizocheza hatua hiyo.
1. Juventus – mabao 10
Kuna ile wanayosema, kama huwezi kumpiga basi uungana naye. Hilo ndilo walilofanya Juventus kwa Cristiano Ronaldo kwa kuamua kumsajili maana amewapiga sana kwenye mechi alizowahi kukutana nao. Katika nyakati zake alizokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid, timu hiyo ilikutana na Juventus mara kadhaa na mara zote Ronaldo alikuwa akiweka mpira kwenye nyavu. Ronaldo amecheza mechi saba dhidi ya Juve na amefunga kwenye mechi zote hizo, akiweka kwenye kamba mabao 10, mabao matatu yalikuwa kwenye hatua ya makundi msimu wa 2013/14, mawili kwenye nusu fainali 2014/15, mawili kwenye fainali 2016/17 na matatu mengine kwenye robo fainali 2017/18.
0 Comments