MAMBO ni moto! Ndiyo unavyoweza kusema ni baada ya viongozi wa Yanga kuweka mikakati thabiti ya ukusanyaji wa shilingi bilioni 1.5 katika kampeni ya uchangiaji wa timu hiyo inayoongozwa na Waziri Anthony Mavunde ambaye pia ni mbunge wa Dodoma mjini.
Fedha hizo zinakusanywa katika kampeni iliyoanzishwa na kocha mkuu wa timu hiyo Mkongoman, Mwinyi Zahera ya kuichangia Yanga kwa mashabiki wake kupitia benki na mitandao ya simu za mkononi.
Kocha huyo, katika kikao chake cha kwanza alichokutana na sekretarieti, wanachama wa timu hiyo walikubaliana kuunda kamati maalum itakayosimamia ukusanyaji wa shilingi bilioni 1.5 zitakazotumika kwa ajili ya usajili wa wachezaji katika msimu ujao wa ligi.
Katika kamati hiyo iliyoundwa na kuongozwa na Mavunde ambaye ni Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, juzi ilikutana na kuanza zoezi hilo la uhamasishaji wa kuchangia fedha hizo na kuweka mikakati yao.
Wajumbe wa kamati hiyo walikutana jijini Dar es Salaam na kuweka malengo ya kukusanya kiasi hicho cha fedha zoezi litakalofanyika kila mkoa. “Zoezi la uchangishaji litaendeshwa mkoa kwa mkoa.
“Yanga imedhamiria kuboresha kikosi chake mwishoni mwa msimu kwa kutimiza ushauri uliotolewa na kocha Zahera. “Katika kikao tulichokutana juzi (Jumapili) tulikubaliana baadhi ya mambo chini ya mwenyekiti wetu Mavunde, kati ya hayo ni kumkusanyia kiasi cha shilingi bilioni 1.5, kocha wetu.
“Fedha hizo aliziomba maalum kwa ajili ya usajili wa msimu ujao na kikubwa kocha anataka kusuka kikosi imara chenye hadhi na kuleta ushindani mkubwa wa ligi na michuano ya kimataifa kama tukifanikiwa kushiriki,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akithibitisha hilo Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema: “Ni kweli kabisa kamati yetu ya uhamasishaji fedha kwa mashabiki wa Yanga ilikutana ili kukubaliana baadhi ya vitu na kuweka malengo hayo, hivyo tusubirie kwanza kwani ndiyo kikao chake cha kwanza.”
0 Comments