MSHAMBULIAJI tegemeo hivi sasa wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere, amesikia taarifa za wao kukutana na TP Mazembe na kutamba ndiyo timu waliyokuwa wanaitaka.
Simba inatarajiwa kuvaana na Mazembe baada ya droo ya juzi iliyochezeshwa ya Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo itakutana na Mazembe katika mchezo wa awali utakaopigwa kati ya Aprili 5 au 6, mwaka huu baada ya kufuzu hatua hiyo kwa kuifunga AS Vita mabao 2-1 katika mchezo wa hatua ya makundi uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kagere alisema kabla ya droo hiyo kupangwa, walijiandaa kukutana na timu yoyote ikiwemo Mazembe.
Kagere alisema wanajivunia ubora wa kikosi chao kinachoundwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa wa kupata matokeo mazuri watakapokutana na Mazembe ambayo ni moja ya klabu kubwa Afrika.
Aliongeza kuwa, hawatarudia makosa waliyoyafanya kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kufungwa idadi nyingi ya mabao ugenini, lengo ni kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali.
“Matarajio yetu yalikuwa ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini tunashukuru tumefanikiwa kufika robo fainali ya michuano hii mikubwa Afrika.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu Mazembe tutakaokutana nao, nafahamu haitakuwa kazi rahisi kuwafunga lakini tutahakikisha tunapambana kufanikisha malengo yetu.
“Hakuna kitakachoshindikana kikubwa ni kuweka malengo kama tuliyoyaweka na kupitiliza, ninaamini ubora wa timu yetu unaweza kucheza na timu yoyote kati ya hizo tatu tutakazokutana nazo na kwa kuanza tutaanza na Mazembe, tunawasubiria,” alisema Kagere.
CHANZO: CHAMPIONI
0 Comments