Kiungo mchezeshaji fundi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ametaja siri ya kiwango chake kikubwa alichokionyesha kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, huku akisisitiza kwamba yeye ni yuleyule wala hajabadilika.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, juzi, Simba ilifanikiwa kushinda mabao 2-1 huku Niyonzima akiwa gumzo kubwa.
Kiungo huyo alitokea benchi katika dakika ya 60 akichukua nafasi ya Mganda, Emmanuel Okwi na kuhusika kwenye bao la pili la ushindi lililofungwa na Mzambia, Clatous Chama baada ya kuuruka kwa makusudi mpira uliopigwa na John Bocco kabla ya bao hilo kufungwa.
Niyonzima alisema aliingia uwanjani akiwa ameona upungufu wa wapinzani wao akiwa benchi.
Niyonzima alisema, akiwa benchi kocha wake alimpa maelekezo ya nini cha kukifanya pindi akiingia na kikubwa alimtaka akae na mpira, kupiga pasi za kwenda mbele ili wapate bao lingine.
“Niwaambie tu watu, Niyonzima ni yuleyule wa zamani hana tofauti na huyu wa sasa, kikubwa ni nafasi tu. Nikiendelea kupata nafasi wataniona zaidi,” alisema Niyonzima.
0 Comments