Wahenga husema “Mkubwa hakosei” hii wakimanisha kila afanyalo mtu mzima huwa sahihi kwa kiasi kikubwa lakini kwa kinachofanyika katika soka la Tanzania usemi huo wa Wahenga umeanza kutiwa doa baada ya wakubwa kuanza kukosea katika wafanyalo.
Katika siku za karibuni kumeibuka na utovu wa nidhamu kwa wachezaji wa vilabu tofauti tofauti kwenye bilinge za TPL.
John Bocco, Abdallah Shaibu Ninja, Juma Nyosso, Benidict Tinocco na Juma Nyangi ni majina yaliyoonyesha utovu wa nidhamu iwe kwa kukusudia au vinginevyo.
Utovu wa nidhamu duniani kote hutokea kuanzia wachezaji, mashabiki na makocha lakini timu yenye mchezaji husika huwajibika kwa faini na mambo kama hayo.
Makala haya yanaangazia namna vilabu vinavyoshiriki moja kwa moja kumuwajibisha mchezaji hata kwa tamko tu.
Alliance FC na Mtibwa Sugar zimeibuka na kutuonyesha upande wa pili wa timu kubwa kwamba wanakosea baada ya wachezaji wao kuonyesha utovu wa nidhamu mara nyingi huwachukia wanaosambaza video fupi kuliko kumuwajibisha mchezaji husika.
Abdallah Shaibu alimpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union kwenye TPL wadau mbalimbali walijaribu kuisambaza video hiyo kujaribu kulaani tukio hilo, na kuikumbusha kamati ya nidhamu kuchukua maamuzi.
Katika hali isiyo ya kawaida Klabu ya Yanga haikutoa taarifa yoyote ya kupinga tukio hilo. Badala yake baadhi ya viongozi na mashabiki wamekuwa wakiwalaumu watu wanaosambaza ujumbe huo. Unaweza kumbuka hata Kelvin Yondani pia alitetewa baada ya kukumbwa na utovu wa nidhamu aliomfanyia mchezaji wa Simba Asante Kwasi.
Msimu wa 2017/2018 John Bocco alimpiga ngumi mchezaji wa Mwadui lakini timu ya Simba haikuonyesha kupingana na tukio hilo, badala yake ikiwasuta waliokuwa wanasambaza video hizo.
Timu kama Alliance na Mtibwa Sugar zimetuonyesha kuwa hata wakubwa hukosea tofauti na imani ambayo wahenga waliijenga kwamba mkubwa hakosei juu ya maamuzi waliyoyatoa.
Klabu ya Alliance imeonyesha ukomavu baada ya mchezaji wake Juma Nyangi kumfanyia Gadiel Michael kitendo kisichokuwa cha kiungwana michezoni.
Kitu cha kwanza walitoa tamko la kupinga tukio hilo lakini pia waliitisha kikao cha Kamati ya nidhamu ya klabu kwa ajili ya kumuwajibisha Juma Nyangi.
Hatua waliochukua Alliance inasaidia kuwatisha hata wachezaji wengine kuepuka tabia za kihuni kama hizo, mfano nchini Italia Mauro Icardi alivuliwa unahodha baada ya utovu wa nidhamu. Kepa Arrizabalaga mlinda mlango wa Chelsea alisimamishwa malipo yake. Yote ni kuepusha kuendelea kwa matukio kama hayo kwa wachezaji wengine.
Mtibwa Sugar pia ilisimama kidete baada ya kipa wake Benidict Tinocco kufanya kitendo kisichokuwa cha kiungwana kwa mchezaji wa Biashara FC huku mwamuzi akiwa hajakiona kitendo hicho.
Mda mfupi baada ya tukio klabu ya Mtibwa iliandika ujumbe wa kulaani tukio hilo. Hii husaidia katika kujenga nidhamu ndani ya timu. Timu kukaa kimya huonyesha kukubaliana na mambo yasiyo yakiungwana kama hayo.
“Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’
Hakika vilabu kama Simba na Yanga hutazamwa kama kioo kwa timu nyingi zinazoibukia inapaswa kuwa mfano wa kuigwa.
Namna vilabu vidogo vilivyochukua hatua kali juu ya wachezaji wao iwe somo na funzo kwa vilabu vya Simba na Yanga kwa sababu hivi ni alama kwa taifa husika.
Sasa kukaa kimya kwa namna yoyote ile pindi utovu wa nidhamu unapotokea kwenye vikosi vyao kunaweza kukaathiri jamii nzima ya soka.
Ndio Alliance wametoa somo, Mtibwa wametoa funzo hali hii haitakiwi kuendelea hivi badala yake kila klabu iwe kinara katika kupinga matukio hayo ili kujenga jamii bora ya soka na ya kuigwa.
0 Comments