Windows

SIMBA YACHUKUA POINTI HIZI KUTOKA YANGA FASTA


BAADA ya hivi karibuni Simba kuwachakaza vigogo Al Ahly na Yanga, jana Jumanne waliendeleza ubabe kwa kutoa dozi kwa mara nyingine kwa African Lyon.

Simba wanaofundishwa na Mbelgiji Patrick Aussems waliendelea ‘kutetema’ baada ya kuwashushia kichapo cha mabao 3-0 African Lyon kwenye mchezo wa kiporo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Huu ni mchezo wa tatu sasa Simba wanapata matokeo mazuri baada ya huko nyuma kuvuna pointi mbele ya Al Ahly kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha ule wa Dar es Salaam Dabi mbele ya Yanga.

Kikosi hicho jana licha ya kutocheza kwa ustadi mkubwa kutokana na mazingira ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid walipata mabao yao kupitia kwa John Bocco aliyefunga mawili na Adam Salamba.

Bocco alifanikiwa kuifungia timu yake bao la kwanza katika dakika ya 28 ya mchezo huo kwa mkwaju wa penalti, huku Salamba ambaye amekuwa hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza, akifunga la pili katika dakika ya 45 baada ya Bocco kupiga shuti kali ambalo lilipanguliwa na kipa wa Lyon naye kumalizia mpira kimiani.

Katika pambano hilo ambalo Simba haikuwa na mastaa wake wawili, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao walibaki Dar kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu, Bocco alifanikiwa kufunga bao lake la saba kwenye ligi msimu huu katika dakika ya 46, likiwa ni la tatu kwa Simba kwenye mechi hiyo.

Kwa sasa Simba wameanza kuinyemelea nafasi ya pili baada ya jana kufikisha pointi 42, zikiwa ni 16 nyuma ya vinara Yanga ambao wamecheza michezo saba zaidi, awali Yanga waliwahi kuwazidi Simba kwa pointi 24 lakini sasa wameonekana kuanza kuzipunguza kidogokidogo.

Hii ina maana kuwa kama Simba wakishinda mechi zao zote za viporo watafikisha pointi 63 na kuwazidi Yanga kwa pointi tano.

Kiwango cha jana cha Simba kwenye uwanja huo kinaonyesha kuwa timu hiyo inaweza kuchukua ushindi sehemu yoyote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Azam ambao jana walitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, ikiwa nafasi ya pili na pointi 50, Ijumaa hii itavaana na Simba kwenye Uwanja wa Taifa na kama Simba wakishinda watakuwa wamepunguza gepu la pointi kwenye nafasi ya pili hadi kubaki pointi tano.

Baada ya mechi ya Azam, Simba watasafiri hadi Iringa kuvaana na Lipuli kabla hawajajiandaa na mechi ya kimataifa dhidi ya JS Saoura ya nchini Algeria.

Pia Mwadui walishinda bao 2-1 dhidi ya Biashara United huku Ruvu Shooting wakitoka suluhu na Kagera Sugar.


Post a Comment

0 Comments