MUDA wa wiki nzima tambo zilikuwa zikitawala kuhusu mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba huku kila mmoja akitamba kuibuka kidedea kwenye mchezo huo.
Hakuna marefu yasiyo na ncha hatimaye Jumamosi tumeshuhudia soka la kitabuni kwa timu zote kongwe pale Uwanja wa Mkapa.
Kama kawaida mechi za watani wa jadi hazikosi matukio na vituko vingi nje na ndani ya uwanja kama ambavyo ilikuwa kabla ya mchezo.
Tumesikia namna ambavyo mashabiki walikesha Uwanja wa Mkapa siku moja kabla ya mchezo kulinda Uwanja kwa kile wanachodai kuhusisha na imani za ushirikina. Yote haya ni mambo ya watani wa jadi.
Dakika 90 zilipokamilika mshindi amepatikana hasa baada ya piga nikupige ya muda mrefu kwa timu zote mbili.
Nikukumbushe kwamba kwenye mchezo huo kipindi cha kwanza hakuna timu ambayo ililenga shuti kwenye lango la mpinzani kwa usahihi zaidi ya kupaisha.
Hii inamaanisha kwamba kila timu ilikamilika idara ya ulinzi ambao ulifanya safu ya ushambuliaji wa timu zote mbili upate taabu kubadili matokeo dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Baada ya kipindi cha pili Simba kupata bao la ushindi kuna watu ambao walibadilika rangi za uso wao ghafla na kupoteza tabasamu lao.
Mchezo wa mpira una matokeo matatu hivyo kupoteza haina maana ya kukufanya upoteze dira ama uwe na hasira kwa ajili ya matokeo ya uwanjani.
Kila mtu alichopanda kwenye mchezo huo ndicho ambacho amevuna hakuna namna nyingine ya kufanya zaidi ya kukubali matokeo na kuanza kujipanga upya.
Mavuno ambayo wameyapata Yanga ndio hayo matokeo, sasa wachezaji na benchi la ufundi wasianze kumtafuta mchawi nani watavuruga mipango yao ya mbele.
Tumeshuhudia namna ambavyo kila timu ilikuwa ikitafuta matokeo na ndio maana ukaitwa mchezo wa mpira.
Matokeo yake huwa hayabadiliki ni yaleyale siku zote, kufungwa, kushinda na kutoa sare mwisho wa ubishi ni dakika 90 uwanjani.
Licha ya kupoteza Yanga walikuwa wazuri uwanjani na wameonyesha afya ya soka na kufanya ushindani kuwa mkubwa kwenye mchezo huo.
Wengi hawakutarajia kuona namna walivyofanya maajabu ndani ya dakika 45 za mwanzo hivyo hakuna timu ambayo si bora kwenye ligi.
Kosa moja walilofanya limewagharimu na kuwapa nafasi wapinzani wao kuvunja ngome yao na kubeba pointi zote tatu.
Mpira ni mchezo wa makosa, kosa walilofanya wapinzani wametumia kwa faida wakaibuka na ushindi wanastahili pongezi.
Kushindwa mchezo mmoja haina maana ya kupoteza michezo yote inayofuata, bado nafasi ipo na mipango inapaswa iendelee.
Imani yangu kwa Yanga ni kwamba wana mwalimu mzuri ambae anajua namna ya kujenga saikolojia za wachezaji wake.
Kwa kikosi cha Simba ambacho kilibeba pointi tatu kinapaswa kiangalie upya namna ya kubaki kwenye ubora huo.
Wasijisahahau kwamba bado hata mzunguko wa pili hawajaanza na timu ambazo wanakutana nazo zina hasira ya kulipa kisasi na kupata pointi tatu hasa kwenye mchezo wa marudio ama zile zilizopoteza awali
.
Kazi kubwa ni kuendeea kupambana kwa ajili ya michezo inayofuata, viporo mlivyonavyo mkivibeza tu kazi itakuwa nzito na kujikuta mnaishia kukumbuka kwamba mliifunga Yanga.
Mafanikio hayaji kwa kumbuka mambo mazuri bali kwa kufanya mambo mazuri zaidi ya yale uliyoyatenda siku za nyuma.
Endapo mtajindanganya kwa mtindo huo anguko lenu litakuwa kubwa tena baya kuliko vile ambavyo mnafikiria.
Mpira wa sasa ni uwekezaji na kujituma katika kila mchezo bila kujali aina gani ya timu mnacheza nayo ushindani unapaswa uendelee siku zote.
Waamuzi pia msijishau katika maamuzi yenu jambo la msingi kuzingatia ni sheria 17 za mpira kwenya maamuzi yenu ili kupata matokeo bora.
Pia mkifanya usawa katika michezo yote itasaidia kuboresha ligi yetu na kufanya tupate bingwa bora kwenye ligi.
Hicho ndicho ambacho tunatarajia kuona burudani ya kweli katika mchezo wa mpira ambao unaendelea kupiga hatua kila siku.
Wachezaji pia kumbukeni kucheza kwa upendo na sio kufanya mpira kuwa vita hakuna kitu kama hicho kwenye ulimwengu wetu wa soka.
Fuateni maelekezo ya mwalimu pamoja na kujituma muwapo ndani ya uwanja ili kupata matokeo chanya, kila kitu kinawezekana.
0 Comments