BEKI mkongwe wa Yanga, Kelvin Yondani 'Cotton' amewaambia Simba waendelea kuchonga, lakini wataonana mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Bara nani ataibuka bingwa.
Kauli hiyo, ameitoa wakati timu hiyo ikiwa kwenye kambini mkoani Mwanza ikijiandaa na mchezo wao wa ligi dhidi ya Mbao FC uliotarajiwa kupigwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga inaongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 58 wakifuatiwa na Azam FC wenye 49 huku Simba wakifuatiwa na 42.
Akizungumza na Spoti Xtra, Yondani alisema; “Sisi hatuna presha kabisa ya ubingwa wa ligi, tunafahamu Simba watateleza na kupoteza michezo inayofuata ya ligi na hilo linawezekana kwao, kwani ngumu kucheza michezo nane bila ya kupoteza.”
“Uzuri wetu sisi tayari tulipata matokeo mazuri katika mzunguko wa kwanza wa ligi na kufanikiwa kukaa kileleni tukiamini mzunguko wa pili utakuwa mgumu, hivyo kila timu itapania kucheza ili zibaki katika ligi zile ambazo zipo katika nafasi mbaya ya kushuka.
“Wao Simba watakutana na kibarua hicho kigumu, hivyo basi hivi sasa tunataka kuona tukipata matokeo mazuri ya ushindi katika michezo ijayo ya ligi na mwishoni mwa ligi tutaona nani bingwa sisi au wao,” alitamba Yondani ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba.
0 Comments