Windows

Wazabuni wa uzoaji taka watakiwa kutoa huduma bora


Na Elinipa Lupembe,Arusha

Wazabuni wa kukusanya takataka katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya Arusha,wilayani Arumeru, wametakiwa kutambua kuwa kazi wanayoifanya ni ya kutoa huduma bora na stahiki kwa jamii na si kujikita na kuweka mbele  zaidi maslahi wanayoyapata.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, alipokutana na wazabuni hao ofisini kwake, mapema wiki hii kwa lengo la kujadili njia bora ya utoaji huduma pamoja na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, hususani katika swala zima ukusanyaji wa taka.

Amesema kuwa, licha ya changamoto nyingi zinazokabili sekta hiyo bado halmashauri inathamini kazi ya huduma zinazotolewa na Wazabuni hao, kwa wananchi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kanuni, sharia na taratibu na kujikita zaidi kwenye makubaliano yaliyomo kwenye mikataba ya zabuni zao.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wote wanaopata huduma ya uzoaji taka katika maeneo yao, kulipia huduma hiyo kulingana na bei elekezi zilizotolewa na kufafanuliwa katika sheria ndogo za kuimarisha Afya na Usafi wa mazingira za Halmashauri hiyo.

“Huduma ya uzoaji taka katika mitaa, inalipiwa si huduma ya bure, niwatake wananchi kutoa ushirikiano kwa Wazabuni wa uzoaji taka pamoja na kutunza taka hizo mpaka pale gari litakapokuja kuzibeba” amesema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo wazabuni hao walizitaja changamoto zinazowakabili katika kazi ya ukusanyaji taka ikiwa ni pamoja na mazingira magumu ya kazi kutokana na changamoto ya ufinyu wa barabara na njia za kungia kwenye baadhi ya mitaa, gharama kubwa za uendeshaji na kutokulipwa kwa wakati na kuthibitisha kuwa, endapo changamoto hizo zitafanyiwa kazi na kulipwa fedha zao kwa wakati itasaidia kutatua changamoto hizo, na kuwawezesha kuzoa taka kwa wakati katika maeneo husika.








Post a Comment

0 Comments