Windows

Simba yapewa siri nzito za Al Ahly

SIMBA ina kibarua kigumu dhidi ya Al Ahly hapo Februari 2 huko Cairo, Misri na baadaye kurudiana hapa nyumbani Februari 12, lakini kama benchi lake la ufundi litapitia kwa umakini rekodi na taarifa za wapinzani wao huenda wakakomaa na Waarabu hao ugenini.
Miongoni mwa mambo makubwa ambayo Simba wanapaswa kuyafanya kwenye mechi hizo dhidi ya Al Ahly ni kucheza kwa umakini wa hali ya juu zaidi katika dakika 30 za mwisho za mechi.
Rekodi zinaonyesha kuwa Al Ahly ambao, wametwaa Ligi ya Mabingwa Afrika mara nane (8) ni tishio zaidi katika muda huo ambao, imekuwa ikiutumia kufunga idadi kubwa ya mabao.
Ingawa pia imekuwa ikifumania nyavu za wapinzani katika dakika nyingine za mchezo, theluthi ya mwisho ya mechi ndio huwa mbaya zaidi kwa timu pinzani ya Al Ahly kutokana na rekodi ya kibabe waliyonayo katika kufunga mabao.
Katika mechi 20 za mwisho ambazo Al Ahly wamecheza kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefunga jumla ya mabao 32 na kati ya mabao hayo, mabao 15 wameyafunga kuanzia dakika ya 61 hadi ya 90 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 46.88 ya mabao yote iliyopachika.
Dakika ambazo zimekuwa zikizaa idadi kubwa zaidi ya mabao ya Ahly ni zile 15 za pili baada ya kipindi cha pili ambazo ni kuanzia dakika ya 61 hadi 75, ambapo timu hiyo imefumania nyavu mara nane ikiwa sana na asilimia 25.
Kwa ujumla Ahly ni tishio zaidi kipindi cha pili kuliko cha kwanza kwani, kati ya mabao hayo 32 ambayo wameyafunga kwenye mechi 20 za mwisho kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mabao 19 (59.38%) wameyafunga kwenye dakika 45 za pili za mchezo huku 13 (40.63%) wakiwa wameyafunga kipindi cha kwanza.
Muda ambao Simba wanapaswa kucheza kwa umakini wa hali ya juu kwenye kipindi cha kwanza ni zile dakika 15 za mwisho kwa maana ya kuanzia dakika ya 31 hadi ya 45 ambazo timu hiyo ya Misri imepachika mabao 6 (18.75%) kati ya hayo 32 waliyofumania kwenye mechi hizo 20 walizocheza hivi karibuni kwenye Ligi ya Mabingwa.
Lakini, pamoja na kutakiwa kujilinda kwa nidhamu kubwa kwenye kipindi cha pili dhidi ya Ahly, Simba ikiwa watashambulia kwa hesabu sahihi katika muda huo, wanaweza kuwashangaza waarabu hao kwani, ndio muda ambao pia wamekuwa wakiruhusu nyavu zao kutikiswa.
Kati ya mabao 13 ambayo Al Ahly wamefungwa kwenye mechi 20 za mwisho za Ligi ya Mabingwa Afrika, nyavu zao zimetikiswa mara nane kipindi cha pili ambapo matatu ni kuanzia dakika ya 46 hadi ya 60, manne kuanzia dakika ya 61 hadi ya 76 huku moja likifungwa dakika 15 za mwisho za mchezo.
Ndani ya Uwanja ingawa mshambuliaji anayecheza kwa mkopo kutoka Huddersfield, Ramadan Sobhi ndiye anayeonekana tishio zaidi kutokana na ubora wake, Simba pia inapaswa kuwatazama zaidi na kuwa makini na washambuliaji Walid Soliman na Walid Azaro.
Azaro, ambaye hadi sasa hajaichezea Ahly mechi yoyote msimu huu na Soliman wamekuwa hawana ajizi katika kufumania nyavu pindi wanapopata nafasi mbele ya lango la timu pinzani.
Soliman (34) anasifika kwa kasi yake ya kuwahi kukaa nafasi sahihi pindi wanaposhambulia, utulivu ndani ya eneo la hatari, kutengeneza nafasi lakini pia ni mfungaji mzuri wa mabao kutokana na mipira ya faulo na penalti.
Kwa upande wa Azaro (23), raia wa Morocco, ana akili ya kuwatoroka na kuwahadaa mabeki, kutumia vyema makosa ya walinzi wa timu pinzani pamoja na kutegeneza.
Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, Azaro na Soliman kila mmoja alifumania nyavu mara sita.
Simba wanapaswa kukomaa kwenye mechi hizo mbili mfululizo dhidi ya Ahly ili iweze kupata mazuri vinginevyo hesabu zao kwenye mashindano hayo zitakwama.
Ratiba zinaibana Simba kwani wakati wao wanakutana na Ahly, AS Vita wanaoshika nafasi ya pili kwenye kundi hilo D wenyewe watakuwa wanakutana na JS Saoura mfululizo hivyo ikiwa watapoteza mechi yao ya mwisho inaweza kutokuwa na umuhimu wowote hata wakishinda. 
Ahly wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi nne hadi sasa, wakifumania nyavu mara tatu huku wakiruhusu nyavu zao kutikisika mara moja wakati AS Vita wenyewe wanashika nafasi ya pili na pointi zao tatu, wakifunga mabao matano na kufungwa mawili.
Simba inashika nafasi ya tatu ikifunga mabao matatu na kufungwa matano huku ikiwa na pointi tatu wakati Saoura wanashika mkia wakiwa na pointi moja wana bao moja la kufunga na manne ya kufungwa.

Post a Comment

0 Comments