Mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile amerejea jana kutoka Misri alipokwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.
Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amesema kwamba Ambokile amerejea baada ya kufanya vizuri katika majaribio yake katika klabu ya El Gounah.
Hata hivyo, Kimbe amesema kwamba pamoja na Ambokile kufanya vizuri katika siku zake sita za majaribio, lakini hawajafikia makubaliano na El Gounah na kwamba dili hilo linaweza kuibuliwa tena Julai.
“Hawa mabwana baada ya kumjaribu kwa siku sita, wakataka kumchukua kwa mkopo, au acheze kwanza kwa miezi sita ndiyo waaamue kumnunua moja kwa moja dirisha kubwa. Lakini sisi tukaona wao kuendelea kuwa naye bila kumnunua ni kuwaminyia nafasi wengine wanaomtaka,” amesema Kimbe
Eliud amerudi wakati mwafaka, kwani Mbeya City wanakabiliwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Mashujaa mjini Kigoma.
0 Comments