Msimu uliopita kabla ya Liverpool kumsajili beki wa kati, Virgil van Dijk, Liverpool ilikuwa inatisha kwa kuwa na safu kali ya ushambuliaji. Hata hivyo, wakati Liverpool ikitupia mabao mengi kutokana na kuwa wafungaji hatari Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane lakini beki yao ilikuwa inapwaya.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alifahamu tatizo lake akaamua kumwaga kitita cha pauni milioni 75 na kumsajili Van Dijk, Januari mwaka jana.
Mwanzoni mwa msimu huu wa 2018/19, Liverpool ikajitosa kumsajili kipa Alisson na tayari Liverpool inafaidi matunda yake.
Liverpool ipo kwenye nafasi za juu za Ligi Kuu England ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Hali kama hivyo inawakabili Manchester United kwani inatisha kwa sasa chini ya kocha wao wa muda, Ole Gunnar Solskjaer, ambapo imeshinda mechi sita mfululizo tena kwa idadi kubwa ya mabao.
Tatizo kubwa sasa kwa Manchester United liko kwenye beki ingawa bahati nzuri ina kipa mzuri, David De Gea.
United imepachika mabao 44 katika mechi 22 za Ligi Kuu England msimu huu, ambapo imezidiwa mabao 15 na Manchester City. Klabu hiyo haina tatizo katika kufunga mabao lakini changamoto ya United ipo kwenye beki kwani i m eruhusu mabao 32.
Man United inahitaji sasa beki imara wa kati, mwenye nguvu, mpiganaji na mwenye uwezo wa kuongoza timu.
Klabu hiyo inasemekana inataka kumsajili beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly, ambaye kwa sifa alizonazo ndio mtu ataifaa Manchester United kurudisha enzi wakati ilipokuwa na ukuta mgumu ulioundwa na mabeki wazuri kama Rio Ferdinand, Nemanja Vidic na Jaap Stam.
Sifa za Koulibaly, ambaye anahesabiwa kama miongoni mwa mabeki bora duniani na anatesa kwenye Serie A ni hizi:
HAPITIKI KIRAHISI
Sifa ya kwanza ya Koulibaly ni kutopitika kwake kirahisi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusoma wapinzani.
Koulibaly mwenye urefu w a mita195, ana uwezo mkubwa wa kupokonya mipira kutoka kwa mastraika wa timu pinzani.
Pia ni mzuri wa mipira ya juu ya vichwa, ambapo anatazamiwa kutengeneza safu nzuri ya ulinzi ya United akishirikiana na Victor Lindelof.
Lindelof aliwahi kukaririwa siku za nyuma akidai anataka beki mwenzake mwenye nguvu kwa ajili ya kucheza naye.
Sasa akiletewa Koulibaly ina maana ndoto ya Lindelof itakuwa imetimizwa na sasa watatengeneza safu nzuri ya ulinzi itakayoweza kukabiliana na washambuliaji wakali duniani.
Koulibaly ni beki mzuri kwa kuwa ni mt u l i v u na ana uwezo mkubwawa kusoma timu pinzani kiasi ambacho atasaidia mastraika kuwa na kazi ya kupachika mabao.
BEKI MWENYE MBIO
Ni shughuli pevu kwa beki yeyote kuchezea timu inayocheza soka la kushambulia kama Manchester United.
Hata hivyo, bado kwa timu inayocheza soka la kushambulia lazima iwe na beki imara.
Pamoja na United kuwa na wachezaji wazuri wa kiungo lakini bado inahitaji beki.
Ni hasa pale inapotokea timu inashambuliwa kwa `counter attack’ ambapo ndio anahitajika beki kwenye mbio wa kuzima mashambulizi.
Koulibaly anasifika kutokana na kuwa na mbio, ambapo atasaidia kwa kiasi kikubwa kwa Manchester United kupeleka mashambulizi kwa timu pinzani bila ya kuwa na wasiwasi kwani watakuwa na beki imara.
KUONGOZA TIMU
Manchester United haina kiongozi kwenye safu yake ya ulinzi kama alivyo Van Dijk kwenye timu ya Liverpool.
Van Dijk anafanya kazi nzuri kama kocha akiwa uwanjani kutokana na mara nyingi kuwahimiza wenzake kuhakikisha wanajipanga na kuwa katika nafasi muafaka kila mara.
Koulibaly amekuwa anafanya kazi kama kiongozi wa timu pale Napoli.
Beki huyu kwanza mwenyewe hujiamini na pia huhakikisha huwapanga wenzake ili kuondosha hatari zote zinazoelekezwa kwenye goli lao.
Koulibaly mara zote hucheza kwa kujituma na mara nyingi huwasukuma wenzake kuhakikisha wanapata matokeo mazuri pale wanapokuwa uwanjani.
Beki huyo alikuwa na mchango mkubwa katika kuisaidia Napoli kufukuzana vikali na Juventus kwenye Serie A msimu uliopita wa 2017/18 ingawa hawakufanikiwa kutwaa ubingwa.
Kama Manchester United itafanikiwa kumpata Koulibaly basi atasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza tatizo lao la kupwaya beki.
0 Comments